07/12/2025
Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ya Somalia imethibitisha uwepo wa mlipuko mpya wa Ugonjwa wa Dondakoo (Diphtheria) ambapo takribani watoto 50 wamefariki huku wengine zaidi ya 1,000 wakiambukizwa.
Katika taarifa yake iliyotolewa Desemba 7, 2025, Wizara imesema watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 15 ndiyo walioathirika zaidi.
Ugonjwa huu hushambulia sehemu za Koo, na huenezwa kwa njia ya hewa, mate au majimaji yanayotoka kwenye sehemu za maambukizi na huambatana na dalili za Kukosa hamu ya kula na kushindwa kula, Vidonda kooni, Kutoa k**asi iliyochanganyika na damu, Utando kwenye koo ambao humzuia mtoto kumeza na hata kupumua, Maumivu makali ya shingo hivyo kumfanya mtoto ashindwe kumeza na kupumua, kupooza sehemu za paji la uso hadi shingoni pamoja na Kifo.
Dondakoo hukingwa kwa Chanjo inayotolewa mara tatu kwa mtoto kwenye umri wa wiki 6, wiki 10 na wiki 14 na kwa Tanzania, hutolewa Bure kwenye Vituo vyote vya Kutolea huduma hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wa umri huu wanapata chanjo ili kuwakinga dhidi ya Ugonjwa huu hatari