06/10/2025
Kitonka Medical Hospital imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuifikia jamii kwa kutoa huduma bora za afya kwa wote, baada ya kufanya ziara maalum katika Kanisa la KKKT Usharika wa New Land, Pugu jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo ililenga kutoa huduma za uchunguzi na ushauri wa kiafya bure kwa waumini na wakazi wa eneo hilo.
Katika tukio hilo lililofanyika siku ya Jumapili, tarehe 5 Oktoba 2025, wataalamu wa afya kutoka Kitonka Medical Hospital walitoa huduma mbalimbali zikiwemo:
Vipimo vya shinikizo la damu (pressure)
Vipimo vya kisukari (blood sugar)
Uchunguzi wa kinywa na meno
Pamoja na ushauri wa kitaalam kuhusu lishe bora na mtindo wa maisha wenye afya.
Huduma hizo zilipokelewa kwa furaha kubwa na waumini wa kanisa hilo, huku wengi wakipongeza juhudi za hospitali hiyo katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa afya mapema.
Akizungumza baada ya huduma hizo, Mchungaji Mkuu wa Kanisa la KKKT Usharika wa New Land – Pugu, aliishukuru Kitonka Medical Hospital kwa moyo wa kujitoa kusaidia jamii kupitia huduma hizo za kijamii. Aidha, aliomba kuwa huduma hiyo iwe endelevu, kwani imeleta manufaa makubwa kwa waumini na imegusa maisha ya watu wengi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Kitonka Medical Hospital alieleza kuwa ziara k**a hizi ni sehemu ya mkakati wa hospitali hiyo wa kukuza afya ya jamii kupitia huduma jumuishi, elimu ya afya, na upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza. Alisisitiza kuwa hospitali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini, mashirika na shule katika kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi.
Kampeni k**a hizi zimekuwa sehemu muhimu ya dhamira ya Kitonka Medical Hospital ya kuhakikisha jamii inakuwa na ufahamu sahihi kuhusu afya, na kuchukua hatua mapema kabla ya magonjwa kuwa sugu