10/03/2025
BIMA YA MAGARI YA THIRD PARTY INAFAIDA GANI KWA MIE NINAYEKATA BIMA?
Ndugu Wasomaji
Kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Bima za Magari Tanzania (Motor Vehicle Insurance Act, Cap.169), kila chombo cha moto lazima kiwe na bima ya utatu (Third party policy). Maana ya neno ni *Third party* ni mtu wa tatu.
*Kwa nini mtu wa tatu?
Ni mtu wa tatu kwa sababu mtu wa kwanza *first party* ni yule mwenye gari. *Second party* ni kampuni ya Bima (Insurer). Hawa ndio wahusika (parties) kwenye mkataba wa bima (contract of insurance). Mtu mwingine yeyote ambaye sio mhusika katika mkataba huo wa bima anaitwa *thirdy party*. Kwa hiyo kwa mfano, *Johnson* ana gari ambalo amekatia bima ya third party kwa kampuni ya *A2Z Insurance Limited*, hapa mkataba wa bima ni kati ya Johnson na A2Z Insurance Ltd. Watu wengine wowote k**a vile dereva, abiria, dereva/mmiliki wa gari jingine au mali iliyopo barabarani ni third party. Hao third party niliowataja hapo ndio walengwa (Wanufaika) wa mkataba wa bima kati ya Johnson na A2Z na sio Johnson mwenyewe wala gari yake. Hivyo, ikitokea gari ya Johnson imepata ajali na kumjeruhi au kumuua mtu yeyote (mfano abiria waliokuwemo ndani ya hiyo gari), hapo abiria ndio watakaolipwa. Au k**a gari ya Johnson iligonga gari ya Jamal na kuiharibu, basi kampuni ya bima ya A2Z italipia gharama za matengenezo ya gari la Jamal na sio la Johnson.
Kampuni ya bima ya A2Z ingeweza tu kulipia gharama za matengenezo ya gari la Johnson (aliyekata bima) na lile la Jamal, iwapo tu Johnson angekuwa amekata bima kubwa (mseto) ambayo huitwa *comprehensive*. Nje ya hapo, Johnson itabidi ajigharamie matengenezo ya gari lake hata k**a gari lake lilikuwa na bima, sababu bima yake ni third party (inamhusu mtu mwingine sio yeye Johnson).
*Sasa basi Kuna faida Gani ya Kulazimishwa Kukata Bima ya Third Party Wakati mimi Mwenyewe Sifaidiki Nayo*?
Huenda na wewe umekuwa ukijiuliza swali hili. Basi jibu ni hili.
1. Bima ya third party imewekwa na serikali kwaajili ya kumlinda mwananchi asiye sehemu ya mkataba wa bima. Ndio maana bima hii ni ya lazima, tofauti na bima ya comprehensive.
2. Kisheria anayesababisha madhara ana wajibu wa kurekesbisha madhara hayo kwa kumlipa fidia yule aliyemsababishia madhara. Hivyo, k**a wewe una gari endapo utagonga mtu au kuharibu mali ya mtu mwingine una wajibika kisheria kulipa gharama ya uharibifu huo uliousababisha.
3. Kwa kutambua kuwa sio kila wakati, mmiliki anakuwa na hela ya kulipia fidia ya hasara serikali ikaweka utaratibu wa bima ili mmiliki anapotakiwa kulipa hiyo bima, kampuni ya bima ndio ilipe.
4. Hivyo, basi bima ya third party inamsaidia mmiliki wa gari lililosababisha ajali kumlipa fidia mtu aliyesababishiwa ajali, badala ya mmiliki kutoa hela mifukoni mwake.
Kwa hiyo, ndio kusema kwamba k**a Johnson alipokuwa akiendesha gari aliligonga gari la Jamal na kusababisha Jamal na abiria wake waumie, na pia gari kuharibika sana. Wajibu wa Johnson ni kumlipa fidia Jamal na abiria wake na kukarabati lile gari. Tuseme kwa mfano gari hasara aliyoipata Jamal ni 5,000,000 na abiria wanatakiwa kulipwa 2,000,000. Basi kiwango hiki cha 7,000,000 kitalipwa na kampuni ya bima badala ya hizo fedha kutoka mifukoni mwa Johnson.
Ni matumaini yangu kwa maelezo haya utakuwa umeongeza uelewa
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote.