13/08/2025
Mzee alileta ujuaji sasa hivi nimejipata ananitafuta anataka nimsaidie, hii dunia ina mambo mengi ya kustaajabisha, na mimi k**a mwanaume siwezi kurudia makosa aliyofanya mzee, ni bora nilee mtoto hata k**a sio wangu kuliko kumtelekeza halafu baadae nipeleke pua yangu eti nataka msaada, hell no.
Iko hivi mzee wangu alimuoa mama akiwa binti mdogo (early 20s), baadae akampa ujauzito akatokomea kusiko julikana akidai ameenda kutafuta maisha, siku zilienda na kwenda mimba inazidi kuwa kubwa na hatimaye ukafika muda wa kujifungua, mama yangu hakuwa hata na akiba ya doti moja ya kanga ndani, alidhalilika sana mpaka kufikia kusaidiwa na wasamalia wema vinguo.
Mama alitembea na vilaka mwili mzima si hilo tu alidhoofika sana kiafya maana alijifungua kwa operation na hakupata matunzo ya aina yoyote hata uji tu ๐ญ.
Ikafika hatua akatoka pale nyumbani na kuhamia ukweni, yaani kwao baba ili angalau tupate msaada hata wa chakula.
Maisha hayakuwa mepesi pale kwa babu, alinyanyaswa kiasi kwamba alijaribu kutaka kujiua mara kadhaa akafeli, kulima ilikuwa yeye, asubuhi mpaka jioni yuko busy na mimi mgongoni, halafu kulikuwa na wanawake wengine (wake wa vijana wa hiyo familia) ambao nao walikimbia wake zao wakaenda kutafuta maisha, kwahiyo ulikuwa ni mji mkubwa na ilionekana k**a kero fulani kwa wao kuishi pale, so mateso yalikuwa makali, kazi za shamba masika na za bustani kiangazi, na hapo hawapewi hata mia ya kujikimu k**a wanawake watu wazima.
K**a baada ya miaka 7 baba yangu alirejea, alirudi na mke mwingine ambaye alikuwa na mtoto mdogo wa k**a miaka 5, akamfikishia kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na mama yangu, tangu amefika hakujisumbua kututafuta wala kwenda kwao kusalimia, ilipita k**a miezi mitatu tangu amefika ndio akawa ameenda kwao kusalimia, alifika na baada ya salamu za hapa na pale mama yangu aliitwa, akaambiwa huyu hapa mwenzio amerudi kusanya matambala yako muongozane, baba akamkatisha babu "mzee mimi nimekuja na mke mwingine na nimemfikishia kule kwangu, sijaja nae kwa makusudi maana naandaa mazingira ili nimlete kumtambulisha mumjue" wakamlaumu pale lakini kwa baadae wakaungana nae.
Lakini wakamwambia lazima uondoke na mzigo wako, nilikuwa mdogo lakini nilikuwa naelewa sana situations.
Kishingo upande baba akaondoka na sisi mpaka nyumbani, njia nzima mama alikuwa analalamika na kulia, huwezi amini tulipofika baba alimwambia mama wewe utakuwa unalala sebuleni na mtoto, sisi tutalala chumbani, ukiona umeshindwa kuvumilia njia ni nyeupe unaweza ukaondoka, shida mama kwao ilikuwa ni mbali sana na pia walikuwa masikini mno ๐.
Alikondeana sana na alichekwa mno na majirani kwa kuishi nyumba moja na mke mwenza wakati nyumba ni chumba kimoja na sebule, si hilo tu yule mke wa baba aliishi k**a mfalme, kazi zote alifanya mama yangu, na alitambiwa na mke mwenzie kila uchwao, uzalendo ukamshinda akaja kuondokaga pale nyumbani, akaenda kijiji cha tatu kutoka tulipokuwa tunaishi.
Hakuwa na nauli, alitembea kwa mguu na mimi nikichoka ananibeba au ananiweka juu kwenye mabega yake, najikaza natembea mpaka tukafika, lakini hakujua anaenda wapi na kwa nani, aliianza tu safari ya imani.
Alipofika kijijini pale aliamua kukaa sehemu, jirani na mji fulani, mchana akaenda kuniombea chakula akijifanya kuna mtu anamsubiri waendelee na safari, kwa bahati nzuri tulikula wote tukanywa maji tukashukuru Mungu kwa siku hiyo.
Tulikaa pale mpaka usiku, ikabidi mwenyeji aulize mbona huyo mtu hafiki, akasema labda amepata matatizo njiani hata mimi nina wasiwasi, tukapewa sehemu ya kulala, usiku tumelala mama akawa ananiambia kila kinachoendelea na kuniomba ushauri, nilikuwa mtoto mdogo sana lakini alifanya hivyo ili angalau ayatoe ya moyoni kwa kujiona ana mtu wa kuongea nae.
Palivyokucha ikabidi aongee ukweli wake wote kwa wale wenyeji na wakaamua kumsaidia, kuna jiko lilikuwepo, wakampa kiwe chumba chake, tukasafisha vizuri tukapewa mkeka na vikoi viwili ndio tukawa tunalalia.
Tulifurahi sana maana ilikuwa ni amani, hata mimi japo nilikuwa mtoto kuna amani fulani nikaanza kuipata, nikaanza kucheza na watoto wengine wakati tulipokuwa kwa baba sikuwa na mood ya kucheza, nachezaje kila muda naona mama analia, mama anafokewa, mama anagombezwa, nilijikuta nakaa around muda wote.
Kulikuwa na mashine za kukoboa mpunga jirani, yule mama aliyetukaribisha kwake akaja kumpeleka mama yangu kwenye hizo mashine kufanya kazi mbali mbali mfano kuanika na kuanua mpunga, kupepeta pumba, na nyingine nyingi ili apate hata 500 ya sabuni, mama alifanya kazi k**a mwendawazimu na kila akipata 5000 anachukua 2000 anampa yule mama aongezee kwenye pesa ya mahemezi ya chakula, elfu 3 anatunza, alikuwa hakosi kuniletea kitu hata k**a ni p**i ya 100 tu, ilimradi nifurahi nisiwe mnyonge.
Alipiga kazi sana, tulikaa pale miaka miwili, akaenda kupanga chumba kimoja, akakodi na shamba hekari moja.
Mwaka ule ule tulipofika kwenye ile familia nilipelekwa kuanza shule, mpaka nafika miaka 7 nilikuwa sijaanza shule ๐ญ, so baada ya mama kupanga na kukodi shamba, hakuacha ile kazi mashineni, aliendelea nayo, tulihamia jirani tu na pale tulipokuwa tunaishi na ile familia ilibaki kuwa ndugu wa karibu, mama alivuna gunia 5 tu za mahindi kwa heka lakini bei ilikuwa nzuri, aliuza zote, akaunganisha na pesa aliyotunza akawa na kiasi kizuri tu cha pesa.
Tukaenda kwa wenyeji wetu akawaaga na nakumbuka siku hiyo ulipikwa ubwabwa na soda za kumwaga, aliwaaga tukaenda kwao mama.
Nilipelekwa shule, mama akawa na biashara ya kuuza nafaka na mafuta ya kula, kwakweli ile biashara iliendelea na nimesoma kupitia hiyo hiyo biashara maana nilisoma hizi shule za kata, ila kwa uchungu niliokuwa nao aisee sikufanya mchezo, nilikaza sana nikafaulu kwa marks za juu kote nilipopita. Mpaka nakuja kutoboa kimaisha haikuwa rahisi hata kidogo.
Mama yangu alikuwa mgonjwa mgonjwa nikampeleka hospital kubwa Dar es salaam, akakutwa na tatizo la moyo, kwamba moyo ulitanuka, lakini nashukuru Mungu lile tatizo liliishaga, niliambiwa msongo wa mawazo na sonona ndio ilikuwa sababu.
Sasa baba yangu mzazi ananitafuta anataka nimsaidie, anasema nimkatie kibali nimpe na mtaji afanye biashara ya mbao, kwakweli bora nionekane hayawani ila kumsaidia mzee siwezi kabisa, maana humo katikati kwenye story yapo mengi sijasema ila nilishawahi kumtafuta kipindi nipo form 2 alichonijibu alisema "wewe hapo ulipo umeshakuwa halafu wewe wa kiume usipende kuomba omba pambana". Nikamwambia napambana vipi na mimi ni mwanafunzi, akajibu, aliyekulipia ada usome ndio unatakiwa umpe matatizo yako yote kuhusu shule ayamalize, nikamwambia lakini baba mbona hunitafuti hata kuniulizia tu ujue hali yangu! Akasema sasa nikishajua hali yako wewe utafaidika na nini? Nilisimama nikaenda kupanda gari, sikujibu neno.
Ushauri wangu kwa wanawake ambao mnaolewa, jitahidini kuangalia na ukoo, ukiona kaka mtu, mdogo mtu, dada mtu, wana matukio ya hovyo ya kufanana usijaribu kuingia kwenye hiyo familia utajuta sana maisha yako yote, ukoo wa kina baba naweza sema baba mdogo na baba mkubwa zangu wote wako hivyo japo viwango vinatofautiana wapo wenye nafuu.
Sasa najiuliza huyu mzee ananiomba msaada ina maana amesahau yote au anatafuta lawama tu?!