27/04/2024
MANENO 9 NA FAFANUZI ZAKE
________________
1.MABADILIKO NI KITU CHA LAZIMA KATIKA MAISHA
Kila kitu kitabadilika bila kujali kwa sasa kipoje.Hata kitu kigumu hubadilika na kuwa laini kadiri muda unavyozidi kwenda mbele.Nyumba imara k**a haiwezi kupewa matunzo hubadilika na kugeuka gofu bila kujali gharama kubwa sana imetumika kuijenga.
Mabadiliko katika maisha hatuwezi kuepuka k**a ifuatavyo
Afya na maradhi,kicheko na machozi,kusifiwa na kukosolewa,kizuri na kibaya,kupata na kukosa,upendo na chuki, kuheshimiwa na kudhalilishwa, uaminifu na usaliti,rafiki na adui, kufanikiwa na kufeli,furaha na huzuni,kupanda na kushuka,usiku na mchana,maisha na kifo.
Chochote chenye mwanzo hakikosi mwisho, sheria za nchi hubadilika,majira ya joto na baridi, uongozi hubadilika, muonekano wa mwili hubadilika,fikra hubadilika.
Hivyo zingatia kwamba hakuna kitu chochote chenye kubaki vilevile milele.
2.HAKUNA CHENYE KUDUMU MILELE
Kila kitu huwa cha kupita,fursa zinakuja na kuondoka, umaarufu unakuja na kuondoka, urafiki unajengwa na kuvunjika,ajali zinatokea,vitu vyenye thamani vinapoteza thamani kwa vitu vipya kuzalishwa,
Mahusiano yako na watu wengine yatabadilika tu.
Mahusiano yako na wazazi wako,mwenza wako, marafiki zako,ndugu zako,watoto wako, wafanyakazi wenzako,wateja wako, wanafunzi wenzako n.k hayawezi kudumu milele.
Mahusiano hubadilika kwa njia tatu
I.Mahusiano hubadilika kwa kutengana
Utatengana na watu kwa sababu wataoa au kuolewa,kupata kazi sehemu nyingine,kuzaa watoto, kusafiri,kurudi masomoni,wengine kuhama makazi
iI.Mahusano kuvunjika
Mabadiliko katika mahusiano yako na watu wengine yanaweza kutokea kwa kuvunja mahusiano nao bila kujali uwekezaji wako kwao ukifika muda wa mahusiano kuvunjika yatavunjika tu kwa sababu wewe sio binadamu wa kwanza au wa mwisho kuwa na mwenza na hauna kinga yoyote ya kuzuia .
III.Mahusiano yako na watu wengine yatabadilika kwa kifo kuwatenganisha.Kifo kitabadilisha mahusiano yako na wapendwa wako nyakati ambazo hauna matarajio yoyote na itatokea kwako k**a ilivyotokea kwa watu wengine na hauna kinga ya kuzuia hilo.
3.HILI NALO LITAPITA
Haijalishi utakuwa na furaha sana au huzuni sana zingatia kwamba hili nalo litapita kwa sababu wewe sio binadamu wa kwanza duniani kupitia hali ambayo unapitia na vilevile huwezi wa mwisho katika ulimwengu huu.
Usiku ukiwa mrefu sana asubuhi huingia na mchana haijalishi utakuwa mrefu sana usiku lazima utaingia.
Kitu chochote kiwe kizuri au kibaya hakiwezi kudumu milele.
Uwe maarufu sana lakini utafika muda wa mtu mwengine kushika nafasi hiyo na uwe mzuri sana utafika muda mtu mwingine anakuja kushika nafasi hiyo.
Jaribu kutazama kwenye kioo je sura yako ya sasa ni ile ya miaka 5 iliyopita?
Hakuna chenye kudumu milele.
Kutarajia vitu kudumu milele ni kutafuta huzuni .
Zingatia kwamba hali yoyote ambayo utakuwa nayo haiwezi kudumu milele.
Umekuwa na furaha sana miaka mingi iliyopita lakini ile furaha bado ipo ?
4.FURAHA NA HUZUNI
Aliulizwa Khalil Gibran kuhusu Furaha na huzuni alisema "Furaha yako ni huzuni yako iliyotoweka.Nyakati ambazo umekuwa na furaha na kicheko zimetokana na nyakati ambazo ulikuwa unatokwa machozi.
Kiwango kikubwa sana cha huzuni huwa ni kiwango kikubwa sana cha furaha ambayo utakuwa nayo baada ya huzuni yako kuondoka.
Ikiwa upo na furaha kubwa sana hivi sasa na endapo ukitazama ndani ya moyo wako utagundua kwamba ni kile kitu ambacho kilikuwa chenye kuumiza sana nafsi yako ndiyo chenye kukupa furaha sana kwa sasa.
Vilevile ukiwa na huzuni kupita kiasi na endapo utachunguza ndani ya moyo wako utagundua kwamba ni kile kitu ambacho kilikuwa kinakupa furaha sana ndiyo chenye kukupa huzuni kupita kiasi kwa sasa.
Furaha na huzuni hatuwezi kuvitenganisha .Vinakuja kwa pamoja na ukiwa na furaha sana huzuni inakaa pembeni inasubiri muda wake na ukiwa na huzuni sana furaha inakuwa pembeni inasubiri muda wake.
Furaha ikija huzuni huondoka na huzuni ikija furaha huondoka na huwa vinapeana zamu na maisha yako yatakuwa hivyo miaka yote .
5.MAISHA HAYANA USAWA
Maisha hayana usawa (life is not fair) zingatia kwamba hakuna usawa katika maisha na hiyo ni asili ya ulimwengu.
Hauwezi kupata kile ambacho unaona unastahili kupata hata k**a upo na sifa na vigezo vyote.
Kwa vyovyote vile itakavyokuwa utakutana na mtu ambaye anamiliki fedha nyingi sana zaidi yako katika umri mdogo sana kwako,kuna mtu atakuwa kipenzi cha watu wengi hata k**a unaona unamzidi sifa,
mtu ataheshimika zaidi yako ,kuna mtu atakuwa na mafanikio makubwa zaidi yako,kuna mtu atakuwa na muonekano mzuri sana zaidi yako,unakuwa kuwa na upendo wa dhati na ukaachwa na mwenza wako, unaweza kujali sana watu lakini usipate upendo wa watu , unaweza kusema watu kwa mazuri lakini wewe unasemwa vibaya,
kufuata taratibu zote lakini hupati nafasi, unaweza kuwa na sifa ya kupata kazi lakini asiekuwa na sifa akapewa nafasi, unaweza kufanya kazi kwa bidii sana lakini mtu mvivu sana akapata mafanikio zaidi yako, unaweza kufanya maamuzi sahihi na ukapata matokeo mabaya sana na mtu mwingine asiefanya maamuzi kwa usahihi akapata mafanikio eneo hilo hilo
Unaweza kula kiafya,kufanya mazoezi,kuepuka pombe na sigara lakini ukapata kansa na uvimbe na mtu mwingine ambaye hayupo makini akaishi kwa furaha na afya tele
Unaweza kufanya kazi kwa bidii sana na ukafukuzwa kazi na mtu mvivu sana akadumu kazini mpaka anastaafu
6.MATATIZO YANATOKEA KWA WATU WOTE DUNIANI
Unafikiri wewe ni nani mpaka usipatwe na matatizo katika ulimwengu huu?
Hakuna binadamu yeyote ambaye yupo na kinga ya matatizo katika ulimwengu huu.
Suala sio kujiuliza KWANINI MIMI badala yake uliza KWANINI ISIWE MIMI
Matatizo hayatazami malengo yako, matatizo hayatazami matarajio yako, matatizo hayatazami afya yako, matatizo hayatazami kipato chako, matatizo hayatazami historia yako, matatizo hayatazami maumivu yako, matatizo hayatazami elimu yako, matatizo hayatazami k**a hauna ndugu au upo nao, matatizo hayatazami k**a upo na ulemavu au upo na viungo kamili,
matatizo hayatazami wewe ni mchamungu au mshirikina, matatizo hayatazami k**a wewe ni muaminifu au msaliti, matatizo hayatazami k**a wewe unasaidia sana au hauna msaada wowote katika jamii,
matatizo hayatazami una na mwenza au hauna, matatizo hayatazami umezaliwa familia ya kimaskini kupita kiasi au kitajiri sana, matatizo hayatazami umesoma maelekezo au haujasoma maelekezo,
7.HAIJALISHI UNAMPENDA MTU MWENGINE KIASI GANI HAUWEZI KUZUIA MAJANGA KUTOKEA KATIKA MAISHA YAKE
K**a kuna mtu ambaye unampenda sana labda mama au baba,wadogo zako au wakubwa zako,mwenza wako, marafiki zako,watoto wako,jirani yako,ndugu zako n.k
Utakuwa unataka kuona wanaishi milele bila kupatwa na matatizo ya aina yoyote ile.
Lakini kiuhalisia ni kwamba jambo hilo haliwezekani kwa sababu hakuna mtu yeyote ambaye yupo na kinga dhidi ya majanga ya huu ulimwengu.
Watu uwapendao ni binadamu k**a binadamu wengine hivyo sheria na kanuni za ulimwengu zinafanya kazi kwa watu wote bila kujali unawapenda sana au hauna upendo nao kabisa.
Watu uwapendao watakumbana na matatizo ya kifedha, kiafya, mahusiano, migogoro kazini,kusemwa vibaya, kukataliwa,kukosa msaada,wapo watafeli shuleni,wapo watafukuzwa kazi,wapo watapewa talaka au kutenda na wenza wao,wapo watapata ajali,wapo watapata kesi mbalimbali,wapo watakuwa na utovu wa nidhamu,wapo watapoteza fedha,wapo watapata ajali,wapo watapoteza maisha katika umri mdogo.
Hauna uwezo wa kuzuia hilo kwa sababu wewe ni binadamu tu k**a walivyo wengine na upo na mipaka na ukomo wa mamlaka .
Hauna kinga ya matatizo wala ndugu zako hawana kinga ya matatizo katika ulimwengu huu.
8. HATUWEZI KUMALIZA MAUMIVU NA MATESO KATIKA HUU ULIMWENGU
Haijalishi utaweka malengo gani, haijalishi utakuja na kampeni gani, haijalishi utaanzisha taasisi au kampini gani,haijalishi utakuwa bilionea leo au baadaye, haijalishi utakuwa profesa leo au siku za baadaye, haijalishi utakuwa mshindi wa tuzo ya Nobel leo au miaka ya baadaye bado haiwezi kumaliza maumivu na mateso kwa watu wote ulimwenguni.
Chochote ambacho utafanikiwa kukipata au utakipoteza hakiwezi kumaliza maumivu na mateso hapa ulimwenguni.
Haijalishi watu watafanya kazi kwa bidii kiasi gani,wafanye ibada kwa kiwango gani,wajiwekee malengo makubwa kiasi gani,wasome vitabu gani,bado haiwezi kuwa guarantee ya kumaliza maumivu na mateso hapa ulimwenguni.
Zingatia yafuatayo
Baadhi ya watu watapata ajali yenye kusababisha ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha,baadhi ya watu watafukuzwa kazi,baadhi ya watu watakuwa masikini lofa wakutupwa,baadhi ya watu watasaliti wenza wao,baadhi ya watu wataugua ugonjwa sugu
-Baadhi ya watu watahukumiwa kifungo cha maisha gerezani,baadhi ya watu watazusha uongo,baadhi ya watu watafilisika,baadhi ya watu watapata maambukizo ya ugonjwa wa virusi vya ukimwi,
-baadhi ya watu watajiua,baadhi ya watu watakuwa na ugumba,baadhi ya watu watakufa katika umri mdogo,baadhi ya watu watapata ujauzito masomoni,baadhi ya watu watabakwa,baadhi ya watu watafanyiwa ulawiti,baadhi ya watu wataacha shule.
Kwa sababu haya ni matukio ya miaka yote tangu utotoni mwako mpaka unaingia kaburini na hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kuyaondoa hapa ulimwenguni.
Uwepo wa matukio hayo ndiyo yanafanya huu uitwe ulimwengu na yataendelea kuwepo matukio hayo ilimradi binadamu wataendelea kuishi hapa ulimwenguni.
9.KAMA KUNA KITU KIBAYA KINAWEZA KUTOKEA KITATOKEA TU NA HAIWEZI KUWA MWISHO WA ULIMWENGU
K**a kuna tatizo lolote linaweza kutokea litatokea tu,hofu haiwezi kuzuia mabadiliko ya huu ulimwengu.
Machozi yako hayawezi kuzuia mvua kunyesha au kujua kuwaka,
Upweke wako hauwezi kuzuia watu wengine kuoa au kuolewa,kufeli masomo kwa mtu yeyote haiwezi kuzuia watu wengine kuendelea na masomo,mtu mmoja kusalitiwa na Mwenza wake haiwezi kuzuia watu wengine kupenda ,mtu mmoja kuacha kazi haiwezi kuzuia watu wengine kuomba kazi ,
Mtu mmoja kuamua kuacha kuzaa haiwezi kuzuia watu wengine kuzaa,mtu mmoja kufunga biashara haiwezi kuzuia watu wengine kufungua biashara
Mtu mmoja kukata tamaa ya maisha haiwezi kuzuia watu wengine kupata hamasa ya kupambana maishani mwao.
Dunia haiwezi kufika mwisho kwa sababu kuna mtu amefilisika au kutajirika,dunia haiwezi kufika mwisho kwa sababu mtu mmoja ameacha kazi au kupanda cheo
Dunia haiwezi kufika mwisho kwa sababu mtu mmoja kusalitiwa na Mwenza wake
Dunia haiwezi kufika mwisho kwa sababu kuna mtu yupo na hasira kupita kiasi juu ya ugumu wa maisha
Mtu mmoja kujuta kwa sababu amesoma lakini haoni manufaa ya kusoma bado haiwezi kuzuia watu wengine kusoma kwa bidii
Yohani Peter
mengi ya kujifunza #