05/10/2025
*Waraka wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania Kuhusu Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025*
*Kauli Mbiu: “Amani Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi”*
*Utangulizi*
Waheshimiwa - Viongozi wa Dini, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Hay-atul Ulamaa, Wagombea wa Nafasi zote za Kisiasa nchini, Waandishi wa Habari na Watanzania wote,
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay’atul Ulamaa) ni taasisi iliyoundwa na wanazuoni wa Kiislamu kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu. Miongoni mwa majukumu yetu ni kutoa nasaha na miongozo ya kiimani na kijamii kwa jamii yetu ili kufikia lengo la kutafuta radhi za Allah na kujenga amani, umoja na mshik**ano imara wa kijamii na kitaifa.
Katika kipindi hiki muhimu cha kihistoria, taifa letu linakabiliwa na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba 2025. Tukiwa na imani kuwa taifa letu linaweza kufanikiwa tu kwa umoja na mshik**ano mkubwa, tunatoa waraka huu k**a nasaha kwa kila Mtanzania na kila mgombea. Lengo letu ni kuhimiza kila mtu kuwa chachu ya amani na haki katika uchaguzi huu.
Waasisi wa Taifa letu hili, walituonesha kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na umoja wa wananchi bila kujali tofauti zao za kidini, kikanda au kikabila. Walitufundisha kuwa taifa lenye ustawi linajengwa kwa haki na huruma, na kwamba hakuna nguvu inayoweza kuvunja taifa linaposhikilia mshik**ano wake.
Sisi tunafuata mfano wao; tusiingize propaganda, chuki, wala ubaguzi wowote - wa kisiasa, kidini ama kikabila -kuvunja umoja wetu na kuharibu maendeleo ya taifa letu hili.
Kauli mbiu yetu “Amani Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi” inaashiria wazi kuwa amani ni kipimo cha mafanikio ya uchaguzi wetu: kabla ya uchaguzi, wote tunajitegemea katika kulinda amani na utulivu wa taifa letu; wakati uchaguzi unafanyika tunahakikisha ufanisi na usalama wa taifa letu unaendelea; na baada ya uchaguzi tunauendeleza mshik**ano na umoja wetu bila kuchelewa.
Tunasema haya bila kupendelea chama chochote au mgombea yoyote, bali tukiamini kuwa amani ni kipaumbele cha juu kwa maendeleo ya nchi yetu na taifa letu.
Kwa misingi hiyo na kwa kuheshimu katiba ya nchi, tunahimiza kila Mtanzania aendelee kutumia haki zake za kikatiba bila hofu. Kwa kuwa viongozi wa dini, hatuhamasishi kuchagua mgombea fulani au chama fulani; badala yake tunaheshimu taifa letu na tunalinda amani na ustawi wake kwa kuhimiza ushiriki salama na wa amani kwa wananchi wote.
*Nasaha na Mawaidha Mema kwa Wagombea Wote na Watanzania*
Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: “Sema: Fanyeni (matendo mema), kwani Mwenyezi Mungu Ataona matendo yenu, na Mtume wake, na Waumini.” (Qur’an 9:105). Aya hii inasisitiza kuwa kila mmoja wetu anawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu kwa matendo yake, na hivyo ni vyema tukakumbuka kuwekeza nguvu zetu katika mema kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na taifa letu.
Uchaguzi huu ni fursa ya kipekee ya kuonesha uwajibikaji na ujasiri wetu katika kuilinda katiba ya nchi yetu. Kila kura ni kipimo cha uhuru wetu na uchambuzi wa matumaini ya taifa letu kuendelea kuwa na amani na ustawi katika nchi yetu.
Tunazungumza nanyi nyote leo, Waislamu na wasio Waislamu, kwa kuwa sisi sote ni sehemu ya taifa moja lenye malengo ya amani, umoja na mshik**ano.
K**a taifa lenye imani na matarajio makubwa, tusahau tofauti za kidini, kikanda na kisiasa na tushike msingi wetu wa umoja na upendo kwa ajili ya kuiendeleza nchi yetu na taifa letu.
Dunia imekuwa ikitupa mifano muhimu katika kipindi hiki: kwa mfano, nchi k**a Malaysia, Indonesia na Morocco zimeonesha thamani ya uchaguzi huru na wa haki. Viongozi wa dini na kijamii huko wametoa wito wa amani na uwazi wakati wa kampeni, huku nchi hizo zikijenga mifumo thabiti ya kulinda haki za wafuasi wa dini zote. Baadhi ya nchi zimeimarisha katiba yake na kulinda uhuru wa dini na haki za wananchi, ikihakikisha uchaguzi unaendelea bila vurugu. Matokeo yao ni funzo kwetu: tofauti zetu za kidini, kikabila, kisiasa na kitamaduni zinaweza kutustawisha badala ya kutuvunja, tukiamini kuwa katiba, uhuru na amani iliyopo nchini ina nguvu ya kutuletea maendeleo.
K**a wanazuoni wa Kiislamu nchini na wananchi wa Tanzania, tuwache ubaguzi wa aina yoyote ile na tuendelee kuenzi thamani za amani na haki katika hatua zote za uchaguzi huu.
*Kwanza: Amani ni Msingi wa Maendeleo na Ustawi*
Hakika amani ni neema kubwa zaidi baada ya imani. Ni upofu wa kimaono kudhani kuwa taifa linaweza kufikia maendeleo ya kweli bila kwanza kuhakikisha wananchi wake wanalindwa dhidi ya vurugu na hofu.
Mipango mikubwa ya kiuchumi na kijamii haina maana yoyote ikiwa inatekelezwa katika mazingira yenye migogoro, ukosefu wa haki na utulivu dhaifu. Amani ni mzizi unaolinda kila mwananchi: mkulima shambani kwake, mfanyakazi kazini kwake, mwanafunzi darasani kwake, na mfanyabiashara sokoni kwake. Ni ardhi ya amani tunayosimama sote juu yake, bila kujali dini, kabila au asili yetu.
Jambo la kwanza tunaloomba kutoka kwenu ni ahadi ya dhati ili kulinda amani na utulivu wa Taifa letu kabla, wakati, na hata baada ya uchaguzi. Jamii inahitaji watu wa maamuzi mema, ambao hawatafanya vurugu pale tofauti zinapojitokeza.
Tunawahimiza wagombea wote, bila kujali vyama vyao, watambue kuwa kiongozi wa kuaminiwa ni yule mwenye dhamira njema ya kulinda na kudumisha utulivu wa taifa.
Katika kipindi chote cha kampeni, ahadi zenu ziwe za kweli, ziwe na mizizi ya dhati katika dhamira zenu, na hatua zenu ziakisi uwazi wa nia zenu. Hakuna nafasi ya udanganyifu au kauli zinazowatia wananchi hofu na wasiwasi.
Amani hutokana na msingi thabiti wa haki, uadilifu na uwajibikaji. Hatua hizi ndizo msingi ambao maendeleo ya kweli yanajengwa juu yake.
Tunasisitiza mambo matatu muhimu:
*a) Vyombo vya Uchaguzi kusimamia Haki na Uadilifu:*
Vyombo vyote vinavyosimamia mchakato wa uchaguzi vinapaswa kuongozwa na misingi ya haki na uadilifu. Hatua zote - kuanzia usajili wa wapiga kura, utoaji wa fomu, upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo - zitekelezwe kwa uwazi, usawa na bila upendeleo. Hili ndilo jukumu la pamoja na uwekezaji wa taifa zima: kuhakikisha kila raia anapata nafasi sawa ya kushiriki uchaguzi huu, huku akiiishi na akihisi amani na uadilifu vimewekwa mbele.
*b) Mchango wa Viongozi:*
Wagombea wote waje mbele na nia safi ya kujenga amani na ustawi wa nchi yetu.
Kiongozi anayestahili kuingia madarakani ni yule anayeonesha uwajibikaji mbele ya Taifa lote, si maslahi madogo ya chama, kabila, au kikundi chake.
Miradi ya maendeleo mnayoisimamia iwe nguzo ya kuwaunganisha wananchi na kuimarisha mshik**ano wa kitaifa, siyo chanzo cha chuki, mgawanyiko au umwagaji wa damu. Endeleeni kushik**ana na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wa uadilifu na uwajibikaji, badala ya kuongozwa na tamaa za kisiasa au maslahi binafsi.
*c) Kuheshimiana na Kuepuka Vurugu:*
Wananchi wote, watumishi wa umma na viongozi tunawajibika kuepuka kila tendo linaloweza kuvuruga amani ya taifa letu. Ni haki kumtetea au kumuunga mkono mgombea unayempenda, lakini haipaswi kufanywa kwa gharama ya kuua matumaini ya wengine. Ushindi wa kweli wa kisiasa haupaswi kupatikana kwa njia ya vurugu, chuki au mashambulizi ya lugha ya chuki, bali kupitia taratibu sahihi, busara na heshima. K**a yanavyotufundisha maadili yetu ya kidini na kijamii, tuujenge mustakabali wa taifa letu kwa misingi ya amani, mshik**ano na ujenzi wa taifa - si kwa uharibifu na fitna.
Mlango wa haki ni mpana na unaleta mbegu za amani na utulivu katika jamii. Kuanzia kutetea haki za mtu aliyedhulumiwa, hadi kulinda haki za kundi zima, tujipange k**a wananchi wa taifa letu hili kuhakikisha hakuna mmoja wetu ananyimwa haki yake. Baadhi ya haki kuu tunazozitambua ni:
*1. Haki ya Kuabudu:*
Kila raia wa Tanzania ana haki ya msingi ya kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa uhuru na bila vizuizi, kwa kutambua kuwa ibada ni chanzo cha maadili bora na mshik**ano wa jamii. Kauli ya Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم: ‘ _Mpeni kila mwenye haki haki yake’ (Hadith)_ inatufundisha kwamba kila mtu anapaswa kupewa nafasi ya kuishi kwa imani yake. Hii ni pamoja na kushiriki katika nyumba za ibada, kufanya sala na maombi kwa amani bila kuingiliwa. Waislamu, Wakristo na waumini wa dini nyingine tunapaswa kusimama pamoja kulinda haki hii, kwa kuwa kuheshimiana katika ibada ni msingi wa mshik**ano wa taifa letu na amani ya vizazi vijavyo.”
*2. Haki ya Kuishi Salama:*
Kila mwananchi ana haki ya kuishi salama na kustawi katika nchi yake bila hatari yoyote ile. Ikiwa mtu yoyote amedhulumiwa haki hii – awe mgombea ama raia wa kawaida – ni wajibu wa vyombo vya dola na jamii kuchukua hatua stahiki. Hatua hizi hazipaswi kuathiriwa na ubaguzi wa aina yoyote ile, kwani haki ni haki kwa kila mmoja. Bila msingi huu wa utu na usawa, hatutaweza kufikia maendeleo thabiti na endelevu tunayoyatarajia katika taifa letu.
*3. Haki za Mwanamke:*
Ni jambo la kusikitisha kuona wanawake wakidhulumiwa au kutukanwa kwa sababu ya majukumu yao ya kisiasa. Katika imani yetu, mwanamke ni mtu aliye na sifa na haki zake katika dini na jamii. Haki zake ni sawa na wanaume. Ni kosa kubwa kumdhalilisha mwanamke yeyote yule; hatuwezi kumruhusu mtu yeyote aeneze chuki au matusi dhidi ya wanawake.
Lazima kukomeshwa kabisa tabia ya kuwatusi wanawake kwenye mitandao ya kijamii au hadharani, na badala yake tukumbatie imani zetu za kuheshimu haki za wanawake na kuwapa nafasi zao za kijamii. Hili ni muhimu kwa amani yetu, kwani dhulma kwa mwanamke inaweza kusababisha vurugu na kuchochea chuki katika jamii.
*4. Haki ya Maiti:*
Hata marehemu ana haki zake kubwa ambazo lazima zitunzwe. Familia yake inastahiki kupata nafasi ya kumzika mpendwa wao kwa haraka na kwa heshima, bila vizuizi visivyo vya lazima. Si haki kuchelewesha mazishi kwa kisingizio cha ada kubwa au urasimu usiokuwa na huruma, kwani kufanya hivyo ni kumnyima maiti haki yake ya mwisho. Ni wajibu wetu k**a jamii kukumbuka kuwa heshima ya mwisho kwa marehemu ni sehemu ya utu wetu wa pamoja.
Kwa hivyo, tuchukue hatua kuhakikisha kila maiti anazikwa kwa wakati na kwa heshima, huku familia yake ikibaki na faraja badala ya usumbufu.
*5. Haki za Waislamu na za Wafuasi wa Dini:*
Waislamu ni sehemu muhimu na isiyoweza kutenganishwa na taifa letu hili, na hivyo wanastahili kufurahia haki sawa k**a raia wengine wote. Ingawa bado yapo madai yetu ambayo hayajatekelezwa kikamilifu, kamwe hatutaruhusu hali hiyo kutugeuza watu wa chuki au kuvuruga mshik**ano wa nchi na taifa letu.
Tunafahamu vyema kuwa chuki na misimamo ya kibaguzi ni sumu inayosambaratisha umoja wa taifa.
Kwa misingi ya imani yetu, Waislamu tutabaki kuwa mabalozi wa amani na maridhiano daima.
Historia ya nchi yetu imetufundisha kwamba utulivu na mshik**ano havikuwahi kutegemea chuki, bali kuheshimiana na kusameheana.
Tunakumbushwa pia hekima ya viongozi waliotutangulia waliotufundisha kwamba tamaa na chuki za kidunia huishia kuleta hasara kwa wote.
Kwa hiyo, tutaendeleza taifa letu na kulinda tunu zetu kupitia mshik**ano uliopo, elimu na uadilifu, tukichagua njia ya haki na ustawi badala ya vurugu na fujo. Amani kwetu ni urithi usio na kipimo, na hatutakubali chochote kiharibu amani tuliyokuwa nayo katika taifa letu hili.
Hata hivyo, mshik**ano na amani haviwezi kudumu bila uadilifu. Uadilifu ndio daraja linalounganisha haki za wananchi wote na utulivu wa taifa. Bila uadilifu, haki hubaki maneno matupu na mshik**ano hubaki ndoto isiyotimia.
*Uadilifu*
Uadilifu ni nguzo ya utawala bora na msingi muhimu wa amani. Bila uadilifu, haki hupotea, ufisadi huota mizizi, na ustawi wa taifa huangamia.
Tunawasisitiza Watanzania kuchagua viongozi waadilifu katika ngazi zote – Urais, Ubunge, Uwakilishi, Udiwani – viongozi wanaojali maslahi ya wananchi kuliko manufaa yao binafsi. Kiongozi mwadilifu huchunga mali ya umma k**a amana, hutoa huduma kwa usawa bila upendeleo, na husimamia sheria kwa haki.
Uadilifu hujenga imani baina ya wananchi na viongozi, hufanya kila raia ajisikie salama na kuthaminiwa, na huchochea mshik**ano wa kitaifa. Taifa lenye viongozi waadilifu ni taifa lenye dira, lenye matumaini, na lenye mustakabali wa amani na maendeleo endelevu. Hivyo basi, tuchague viongozi wanaoweza kusimama imara mbele ya vishawishi, wanaosema kweli na kutenda kwa haki, ili Tanzania ibaki kuwa mfano wa kuigwa kwa majirani na dunia nzima.
*Pili: Maadili ya Ushindani wa Uchaguzi*
Uchaguzi ni njia ya kistaarabu na ya kisasa ya kusimamia amana ya wananchi na kuchagua viongozi wa kuwatumikia.
Ni mwendelezo wa utekelezaji wa matakwa ya Katiba yetu ya nchi, na siyo chanzo cha migogoro wala uhasama baina ya watu na vyama vyao. Ili uchaguzi uzalishe matunda ya kweli na kheri kwa taifa, ni lazima ufanyike chini ya mwanga wa maadili mema na busara.
Tunapenda kusisitiza misingi ifuatayo:
*a) Ukweli katika Ahadi:*
Ahadi za kampeni si maneno mepesi ya kupumbaza watu, bali ni mikataba mbele ya Mwenyezi Mungu na wananchi. Ahadi zenu ziwe za kweli, za kutekelezeka, na ziwe na lengo la kulinda maslahi ya taifa. Mwananchi mwema hatamki uongo, na viongozi waadilifu hawatadanganya watu wao. Ahadi zenu zikumbukwe k**a nyenzo za kujenga, si za kupoteza matumaini. Kila neno lenu liwe na uzito, na kila tangazo la kisiasa litekelezeke kwa vitendo.
*b) Lugha ya Kistaarabu:*
Tunawasihi wagombea wote wainue hadhi ya lugha ya kisiasa. Epukeni kabisa matusi, kashfa, kejeli, uvumi na maneno ya uchochezi.
Tanzania imejengwa juu ya undugu, mshik**ano na heshima; tusikubali maneno yasiyo na staha yagawanye taifa letu. Lugha yenu iwe ya kuleta matumaini, ya kuelekeza maono na suluhisho, si ya kuumiza mioyo au kupandikiza chuki.
Kila neno liwe ni daraja la mshik**ano, si ukuta wa kugawa watu na taifa letu.
*c) Ushindani kwa Sera:*
Msingi wa ushindani wa kisiasa ni hoja na sera, si shutuma au ubaguzi. Wananchi wanatarajia kuona wagombea wakitoa dira za maendeleo, mipango thabiti, na suluhisho makini kwa changamoto za taifa. Hoja zenu ziwe za kuimarisha uchumi, kulinda haki za kijamii na kukuza mshik**ano wa taifa letu. Uchaguzi bora ni ule unaotupatia viongozi waadilifu na wabunifu, si wa kulaumiana na kudhalilishana.
*d) Kuepuka Habari Bandia na Uvumi:*
Vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, na kila mwananchi wanalo jukumu la kusambaza ukweli pekee. Habari za uongo, uvumi, na propaganda ni sumu inayoweza kusababisha hofu na kuvuruga amani yetu. Tunahimiza watoa habari wote kuhakikisha taarifa mnazozitoa ni za kweli, zenye ushahidi na nia njema. Uandishi wa habari uwe chombo cha kuelimisha na kujenga mshik**ano, si silaha ya kuchochea fitina na uhasama.
Ukweli ni ngao ya amani, na uongo ni chanzo cha maafa.
*Tatu: Maadili ya Uongozi wa Umma*
Nafasi yoyote ya umma, iwe ni Urais, Ubunge, Uwakilishi ama Udiwani, si fursa ya kujinufaisha wala kujivunia, bali ni amana kubwa na jukumu zito la kutumikia wananchi.
Mafanikio ya kiongozi mwenye hekima hutegemea msingi wa uadilifu, huruma na uongozi wa busara.
Tunasisitiza:
• *Uadilifu kwa Wote:* Uadilifu ndio msingi wa utawala bora.
Kiongozi anawajibika kutenda haki kwa raia wote bila ubaguzi wowote.
Kwa kuwa mwadilifu, anahakikisha kila mtu anapata haki sawa na anahisi ni sehemu ya taifa letu.
• *Huruma na Upendo:* Uongozi sahihi ni kuwahudumia wananchi na kulinda maslahi yao, hususan wanodhulumiwa, wanyonge na masikini. Kiongozi wa kweli ni yule anayehisi maumivu ya watu wake na anakesha kwa bidii kuhakikisha wanapata msaada.
Huu ndio uongozi wa mfano unaojengwa juu ya misingi ya uadilifu, huruma na kujitolea kwa dhati; uongozi unaoweka mbele maslahi ya taifa na watu wake kuliko manufaa binafsi.
*• Ushauri na Majadiliano:* Taasisi za dini na wananchi hushauriwa kupanga masuala ya taifa kwa hekima.
Tunawahimiza viongozi kusikiliza hoja na maoni mbalimbali – kutoka kwa wataalamu, viongozi wenzao, na makundi ya kijamii. Maamuzi yanayojengwa juu ya ushauri yanakaribia usahihi na ni rahisi kukubalika na wengi. Kuchukua Ushauri na kufanya majadiliano inatujengea njia thabiti: kwa pamoja tunapata uamuzi sahihi na kuimarisha mustakbali wa nchi na taifa letu.
*Hitimisho na Wito*
Tunawasihi nyote – Wagombea, Viongozi wa Dini, Vyombo vya Habari, Taasisi za Kiraia na Watanzania wote – kuchukua uchaguzi huu kuwa fursa ya kuimarisha umoja wetu wa kitaifa na kuonesha mfano wa ustaarabu katika ushindani wa kisiasa.
Kumbukeni kuwa vyeo hupita, lakini taifa linabaki; matendo yetu sasa yatakuwa mfano kwa vizazi vijavyo. Tunawaomba nyote kuwa mabalozi wa amani: tushirikiane, tuue chuki, na tushik**ane katika maono ya ujenzi na maelewano kwa taifa letu.
Tunatoa wito maalum kwa vyombo na taasisi zifuatazo kuhakikisha mchakato wote wa uchaguzi unafanyika kwa amani na haki:
• *Viongozi wa Dini:*
Endeleeni kuwaunganisha waumini wenu kwa dua, maombi na mafundisho ya amani. Tumieni mahubiri na mikutano ya kidini kuimarisha hisia za upendo na uwajibikaji miongoni mwa waumini wenu. Kamilisheni harakati za maelewano kati ya taasisi na dini tofauti; epukeni kabisa maneno ya kuchochea chuki au ubaguzi katika nyumba za ibada.
• *Vyombo vya Habari:*
Ripoti masuala ya uchaguzi kwa uadilifu na uwazi.
Epukeni kusambaza habari za uongo, uvumi, au maneno ya kichochezi.
Endeleeni kuwa vituo vya ukweli na taarifa za ujenzi wa taifa letu.
Badala ya kusababisha hofu, saidia kuongeza uelewa na umoja miongoni mwa wananchi.
Chora picha nzuri ya mustakbali wa taifa letu kwa kutafuta ukweli na kuufikisha kwa umma kwa busara.
• *Taasisi za Kiraia (NGOs na Mashirika ya Jamii):*
Shirikisheni elimu na uhamasishaji kuhusu kulinda katiba ya nchi na haki za kiraia.
Endeleeni na kampeni za kuelimisha wapiga kura kuhusu umuhimu wa uchaguzi salama, wa amani na uwajibikaji.
Pambana dhidi ya upotoshaji wa habari na mipango ya kuchochea ghasia: elimu mnayoitoa ni muhimu katika kudumisha haki na amani.
• *Wananchi Wote:*
Tuungane na tujenge ulinzi na usalama wa umoja wetu. Tuwe waangalifu dhidi ya uvumi na uongo usiotokana na ukweli; badala yake, tushirikiane kutafuta haki na maendeleo ya taifa letu. Kuchagua kiongozi mwenye kheri ni jukumu letu kubwa; tukumbuke kwamba nguvu kubwa ya taifa letu iko katika umoja na utu wetu kwa pamoja.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Aihifadhi nchi yetu ya Tanzania dhidi ya kila fitina, na Atuongoze sisi sote katika kila hatua ya uchaguzi huu.
Tunamuomba Atupe viongozi wenye hekima na uadilifu ili kuliongoza taifa letu kwa faida ya Umma wote.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Atuongezee nguvu ya amani na hekima katika serikali ijayo, ili tuendelee kufuata misingi ya utawala bora na kulinda haki za Watanzania wote.
Mwenyezi Mungu Ndiye Mwezeshi.
*Imetolewa na:*
Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (HAY’AT ULAMAA)