23/06/2025
🎙Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Manyara, Bahati Haule, imesema wameanza rasmi kufuatilia sakata la kipa wa Fountain Gate, John Noble aliyesimamishwa na klabu yake kwa tuhuma za kucheza chini ya kiwango dhidi ya Yanga SC.
Haule amesema ofisi yao haijapata rasmi malalamiko yoyote juu ya mchezaji huyo, lakini baada ya kusikia mitaaani kuwa kuna mazingira ya rushwa yaliyotumika kwa golikipa huyo hadi kusababisha kufungwa mabao ya uzembe, wameamua kufuatilia.
" Ni kweli hata sisi tumesikia kuwa magoli aliyofungwa huyo kipa yalikuwa na utata kwamba bao la kwanza alipigiwa shuti dogo akatema mpira kwa uzembe na goli la pili alirudisha mpira golini," amesema Haule.
Amesema wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya Takukuru kifungu cha 15 kilichofanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bungeni Mwaka 2024.
" Sheria hiyo imeongezewa suala la kuwa rushwa ya uchaguzi, rushwa michezoni, kamari, michezo ya kubahatisha na mambo ya burudani," amesema Haule.
Alisema vijana wa Takukuru hivi sasa wapo kazini kuchunguza suala hilo kwani baada ya kusikia malalamiko katika baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii wameanza uchunguzi.
Alisema watatoa taarifa rasmi ya suala hilo mara baada ya uchunguzi kukamilika na hatua zaidi kuchukuliwa juu ya suala la mchezaji huyo.
Noble anatuhumiwa kucheza chini ya kiwango katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Aprili 21, 2025 na kuchangia timu yake ya Fountain Gate kufungwa mabao 4-0 dhidi ya Yanga SC.
Cc: Mwanaspoti