24/10/2025
MGANGA MKUU WA SERIKALI AIPA KONGOLE HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA AMANA KWA HUDUMA BORA ZA AFYA
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amefanya ziara ya siku moja Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana kwa lengo la kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma za afya pamoja na kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo.
Dkt. Magembe amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokidhi viwango na kwa wakati.
Aidha ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo na kuwataka wataalam kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kufanya hivyo ni kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nimeona moyo wa kujituma miongoni mwa watumishi, na hii ni alama ya uzalendo na weledi, nawasihi muendelee kuzingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na mshik**ano miongoni mwenu ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi” amesema Dkt. Magembe
Kwa Upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Dkt. Bryceson Kiwelu, alitumia fursa hiyo kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha hivi karibuni ambapo ameeleza kuwa hospitali imefanikiwa kuboresha mifumo wa TEHAMA, kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu, na kuimarisha huduma za dharura.
Katika ziara hiyo Dkt. Magembe ametembelea baadhi ya maeneo ya kutolea huduma ikiwemo Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Radiolojia, pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo amepata nafasi ya kuzungumza na wananchi na kusikiliza maoni yao juu ya huduma wanazopatiwa hospitalini hapo.