01/03/2026
๐ก๐๐ ๐ฅ ๐ฌ๐ฎ๐๐ผ๐ฎ ๐ ๐ฎ๐๐ผ๐ธ๐ฒ๐ผ ๐๐ฎ ๐จ๐๐ฎ๐ณ๐ถ๐๐ถ ๐๐๐ผ๐ป๐๐ฒ๐๐ต๐ฎ ๐ ๐๐ฒ๐น๐ฒ๐ธ๐ฒ๐ผ ๐ ๐ฝ๐๐ฎ ๐๐ฎ ๐๐๐ท๐ฒ๐ป๐ด๐ฎ ๐จ๐๐๐ฎ๐ต๐ถ๐บ๐ถ๐น๐ถ๐๐ ๐๐ต๐ถ๐ฑ๐ถ ๐๐ฎ ๐ ๐ฎ๐ด๐ผ๐ป๐ท๐๐ฎ ๐๐ฎ ๐ ๐น๐ถ๐ฝ๐๐ธ๐ผ ๐ฌ๐ฎ๐ป๐ฎ๐๐ผ๐๐ฎ๐ฏ๐ฎ๐ฏ๐ถ๐๐ต๐๐ฎ ๐ป๐ฎ ๐ช๐ฎ๐ฑ๐๐ฑ๐ ๐๐ต๐๐ฟ๐ถ๐ณ๐
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), tarehe 26 Februari 2026, kupitia mradi wa RAFT (Resilience Against Future Threats through Vector Control), imewasilisha matokeo ya utafiti kuhusu magonjwa ya mlipuko yanayoenezwa na mbu pamoja na usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu, hatua inayolenga kuimarisha ustahimilivu wa taifa katika kukabiliana na vitisho vya magonjwa hayo.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Tafiti, Dkt. Nyanda Elias Ntinginya, amesema Tanzania inahitaji kuimarisha mifumo yake ya ufuatiliaji na maandalizi ili kukabiliana kwa ufanisi na ongezeko la vitisho vya magonjwa yanayoenezwa na mbu.
Amesisitiza kuwa tafiti za kisayansi zinapaswa kuwa msingi wa maamuzi ya kisera, hasa katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya mazingira, ukuaji wa miji na ongezeko la mwingiliano wa watu vinaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa k**a dengue na magonjwa mengine ya virusi yanayoenezwa na mbu.
Kwa upande wake, Mtafiti Kiongozi wa Mradi wa RAFT, Dkt. Alphaxard Manjurano, amesema lengo la mkutano huo lilikuwa kuwasilisha matokeo muhimu kuhusu usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu na vitisho vya magonjwa ya mlipuko yanayoenezwa na mbu, pamoja na kuyajadili kwa kina na wadau wakuu wa udhibiti wa wadudu dhurifu nchini.
Akiwasilisha matokeo ya tathmini ya kitaifa ya utayari wa mfumo wa afya kukabiliana na vitisho vya mbu, Dkt. Manjurano alibainisha kuwa licha ya kuwepo kwa vituo 34 vya ufuatiliaji wa malaria (sentinel sites), bado kuna haja ya kuanzisha programu mahsusi ya kitaifa ya ufuatiliaji wa kawaida wa mbu wanaoeneza magonjwa.
โKwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2024, ufuatiliaji wa mbu wa kuanzia hatua za mabuu hadi mbu waliokomaa haujawahi kufanyika kwa mfumo wa kitaifa. Hii inaonesha umuhimu wa kuimarisha mfumo wa utambuzi wa mapema wa hatari za milipuko ya magonjwa ya yanayoenezwa na wadudu,โ alisisitiza Dkt. Manjurano.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya kupitia Programu ya Taifa ya Udhibiti wa Malaria, Bw. Winfred Mwafongo, amesema matokeo hayo yatasaidia kuboresha sera na miongozo ya kukabiliana na malaria na magonjwa mengine yanayoenezwa na wadudu.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Jovin Kitau, ameipongeza NIMR kwa kufanya utafiti huo, akisema utachangia kuimarisha kinga ya jamii dhidi ya magonjwa yanayoenezwa na wadudu na kuongeza usalama wa afya ya umma.
Aidha, Mtafiti Mkuu kutoka NIMR, Dkt. William Kisinza, amesema katika majadiliano ya kikao hicho wadau wamependekeza kuimarishwa kwa programu maalumu inayosimamia masuala ya wadudu dhurifu ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa magonjwa yanayoenezwa na wadudu.
Kwa upande wake, Bi. Jackeline Martin, Mtafiti kutoka NIMR aliyefanya utafiti kuhusu ufanisi wa viuatilifu vilivyopo kwenye vyandarua, amesema matokeo yanaonesha ongezeko la usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu hivyo, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuboresha mikakati ya udhibiti ili kuhakikisha vyandarua vinaendelea kuwa na ufanisi.
Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Protea, jijini Dar es Salaam, uliwakutanisha wadau mbalimbali wa udhibiti wa wadudu dhurifu kutoka Wizara ya Afya, NIMR, Shirika la Afya Duniani (WHO), Taasisi ya Afya ya Ifakara, pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya.
.