20/11/2017
MAISHA NI SAWA NA UKUAJI WA MMEA
Wengi wetu huongelea mafanikio katika nyanja zote za maisha.
Ukimuuliza kijana yeyote njozi zake ni mafanikio tu!
Kila mtu hupenda mafanikio na maisha ya raha na furaha daima.
Hata hivyo pamoja na kutaka mafanikio bado wengi hawavifikii vilele vya mafanikio kwa sababu hawazingatii kanuni za msingi za mafanikio, iwe katika ndoa, biashara, elimu, uongozi, utumishi, na mengineyo.
Hebu leo tuangalie kanuni chache za mmea kufikia kilele cha mafanikio;
Shambani mwangu niliipanda punje moja ya mahindi. Baada ya siku chache ilivimba na hatimaye polepole ikachipua kwa kuipasua ardhi.Nilipoiangalia kwa makini niliona siku si nyingi punje ile imeoza na kuishia kabisa. Ndipo nikashangaa sana kuona mche mwororo umechipia na ghafla ukakua kufuatia mvua zilizoendelea kuunywesha maji.
Ngoja nikuambiae ndugu unahitaji mvua ili uweze kufanikiwa.
Unahitaji watu wa kuchochea kufikia kilele cha mafanikio yako!
Mche huo ulipitia hatua kadha wa kadha hadi kufikia kimo cha kuzaa.
Mche huu hata hivyo ulikabiliwa na wadudu waharibifu na ulikuwa ukiharibiwa mara nyingi na kudhoofu sana lakini uliendelea kuvumilia na haukuacha kutoa majani mapya baada ya siku si nyingi za mashambulizi.
Sikiliza maadui ni sehemu ya hatua ya kufikia mafanikio yako... Ustawi wa mmea uliwavutia wadudu ili waushambulie!
Wakati mwingine mvua zilizidi sana na mmea badala ya kukua ulidumaa siyo hivyo tu bali pia jua lilipozidi sana ulikaribia kukauka.
Yote hayo yalikuwa ni mapito ambayo mche huu ulipaswa kuyapitia ili kufikia kilele cha mafanikio.
Hatimaye miezi ikaenda na ndipo mmea huu kwa mara ya kwanza ulionekana umeweka mbelewele na kwa pembeni ukiwa umebeba matunda.
Ulionekana kunawiri na hata wapita njia waliutamani hata wakadhani mmea huu ulikuwa haujapitia shida ya uhaba wa mvua, wadud,ukungu, jua kali na ardhi isiyo na rutuba.
Mkulima aliutunza kwa matazamio makubwa.
Kumbuka katika magumu yote haya mkulima anautunza mmea...yaani Mungu!
Na sasa twashuhudia makumi mengi ya punje yakiwa yamepangwa kwa ustadi mkubwa. Iwapo tulipanda mbegu moja lakini sasa tumevuna mamia ya punje kwa hakika hiki ni kilele cha mafanikio kwa mmea huu.
Lakini cha ajabu huu mmea umetoa vyote kwetu na haukuwa na choyo ulipofikia kilele cha mafanikio.
Cha ajabu mmea huu ulikubali kufa ili uvunwe na kutoa mazao yake yaliyokomaa.
Huu mmea haukuwa mbinafsi hata ulipofikia kwenye kilele cha mafanikio.
Mbegu yenyewe ilikufa huko ardhini na haikuonekana tena, nauliza iko wapi mbegu niliyoipanda mwanzoni na imekuwaje nimeipoteza milele na kuipata ikiwa makumi mengi?
Katika kufikia kilele cha mafanikio wakati mwingine kubali kupoteza, sikiliza hupotezi bali unawekeza!
Kubali kupitia hatua za changamoto na magumu. Punje ililazimika kupasua ardhi ili itoke. Ni kweli punje ingekata tamaa ingebaki ardhini lakini ilijipa moyo ikapenya kwa nguvu kubwa. Kubali kukumbana na magumu maana hayo ndo yatakufanya unekane baada ya kuyavuka! Usikimbie magumu utabaki chini siku zote!
Ikiwa ningeihitaji sana napo ningekuwa sina hekima maana imenishuhudia kwa kunipa zaidi ya matarajio yangu.
Watu wengi wanang'ana na vitu vyao vya zamani wakidhani vitawatoa tu.
Sikiliza ipo namna mpya na mwanzo mpya haijalishi umekuwa mhanga kiasi gani. Uchumi wako, elimu yako na hata utumishi wako umebaki ardhini kwa sababu hutaki kuupoteza umimi. Kila kitu unachokifanya unatanguliza "umimi" acha ni lazima umimi ufe...huo ubinafsi sharti ufe ndipo waweza kuinuka kufikia kilele cha mafanikio.
Kaka na dada mafanikio ya kweli yamejengwa Juu ya Kanuni bora sana za kimbingu k**a ulivyo ukuaji wa mmea.
Amka uanze sasa haujachelewa rafiki yangu.
Mafanikio ya kweli ni kanuni halisi za kimbingu zisizobadilika.
Mungu anaona juhudi zako k**a anavyouangalia mmea unapopambana kufikia kilele cha mafanikio. Anza sasa, mafanikio yako ni ya hakika katika nyanja yoyote!
Ni Rojorojo natural remedies na mtumishi William!