12/05/2017
TATIZO LA KUTOKWA NA HARUFU MBAYA MDOMONI
Tatizo la kunuka kinywa, huwasibu watu wengi, na huwa kero
kubwa kwa waliokaribu na mwenye tatizo hili. Mara nyingi mwenye tatizo hili huwa hafahamu, na wengi huona vibaya kumweleza mtu mwingine kuwa kinywa chake kinatoa harufu. Na wenye tatizo hili pia wakifahamu hupata mfadhaiko sana wa mawazo, na kutopenda kuongea kwenye kusanyiko la watu kwa kuhofia kuwakera wanaomsikiliza. Tatizo hili linaweza kupatiwa ufumbuzi iwapo mwenye tatizo atafahamishwa na hivyo kutafuta tiba stahiki.
Kunuka kinywa ni nini?
Harufu mbaya kutoka kinywani hutokana na kutoa pumzi inayonuka vibaya ambayo huweza kunuswa na wanaokuwa karibu na mwenye tatizo hili. Pia hii hujulikana kwa lugha ya kigeni k**a “halitosis”. Harufu hii inaweza kutokea mara kwa mara, au inaweza kudumu kwa muda mrefu, kutegemeana na chanzo chake.
Dalili za kutoa harufu mbaya kinywani
Dalili za kuwa na harufu mbaya kinywani huwa zinahisiwa na wale wanaokuwa karibu na mwenye tatizo hili. Mwenye tatizo hili mara nyingi anakuwa ameshaizoea ile hali, hivyo hawezi kuhisi hiyo harufu. Harufu hii huwa kero kwa waliokuwa karibu, wakati mwingine unaona k**a watu wanagusa-gusa pua zao, wanasogeza nyuso zao mbali au kuonyesha kwa mbali (bila kuwa dhahiri sana) dalili ya kukunja uso k**a wanakerwa na jambo fulani.
Chanzo cha harufu mbaya kinywani na dalili zake
Harufu mbaya kinywani inaweza kusababishwa na
Tatizo kinywani au
Tatizo nje ya kinywa
Vyakula au vinywaji vinavyoacha harufu kinywani
Chanzo cha kufikirika (psychological)
Tatizo la hisia tu (kufikirika tu bila kuwa na uhalisia)
1. Tatizo kinywani
Kinywa ni makao ya mamilioni ya bakteria ambao hukaa k**a makazi yao, na sehemu kubwa wanakopatikana kwa wingi ni kwenye ulimi. Bakteria hawa huwa chanzo kikubwa cha harufu mbaya kutoka kinywani kwa watu walio wengi. Kwa kawaida kinywa huweza kutoa harufu ambayo siyo ya kukera, na inakubalika kuwa ni ya kawaida, mfano asubuhi kinywa hutoa harufu ambayo huondoka mara moja baada ya kupiga mswaki au hata kusukutua kwa maji tu. Harufu hii hutokana na kuwa unapokuwa umelala, na kinywa kimefungwa, mate hupungua sana kinywani, hivyo hufanya mazingira haya kuwa mazuri kwa bakteria kuzaliana na kuongezeka kwa kiwango kikubwa na pia kutoa muda kwa bakteria kumeng’enya mabaki ya chakula kinywani na kuleta harufu mbaya kinywani. Hali hii huwa tofauti wakati wa mchana, maana mate hutengenezwa kwa wingi katika hali ya kawaida na kusaidia kusafisha na kuondoa mabaki ya chakula, na kuzuia harufu kinywani.
Harufu hii ikianza kuwa mbaya na ya kukera watu wengine karibu yako ndipo huangaliwa k**a tatizo linalohitaji matibabu. Harufu inayodumu kuwa mbaya na ya kukera huweza kusababishwa na
1.1 Chanzo: Ugonjwa wa fizi
Picha hii inaonyesha ugaga (dental calculus) na ugavu (dental plaque) uliotanda kwenye meno karibu na fizi, na fizi zilizoshambuliwa na kulika kutokana na ugonjwa wa fizi
Ugonjwa wa fizi husababishwa na utando wa uchafu unaoitwa ugavu (dental plaque). Uchafu huu ukiongezeka kwa wingi, husababisha ufizi kushambuliwa, kupoteza ubora wake na kuwa laini, mishipa midogo ya damu kwenye fizi huwa na vidonda vidogo vidogo (ulceration) na kuvuja damu kwa urahisi, fizi zinaachia nafasi kati yake na jino, chakula kinakaa, na pia fizi husinyaa (hurudi nyuma) na kuacha wazi sehemu ya jino inayopaswa kufunikwa na hivyo kuleta ukakasi wa meno. Ugavu ukikaa kwa muda mrefu bila kuondolewa hutengeneza ugaga (dental calculus). Ugavu (dental plaque) huwa na mamilioni ya bakteria, ambao humeng’enya mabaki ya chakula na kusababisha harufu mbaya kutoka kinywani.
Dalili:
• Ufizi kutoa damu kwa urahisi ukiguswa na kitu chochote hata mswaki, kutafuna vitu k**a mkate mkavu, mua, matunda k**a peasi, mapera n.k.
• Usaha kutoka kwenye fizi kati ya meno, au uvimbe wenye usaha pembeni ya jino
• Meno kulegea kutokana na mfupa unaoshikilia jino kumomonyoka kwa ndani
• Harufu mbaya kutoka kinywani
1.2 Chanzo: Ugonjwa wa kuoza kwa meno
Picha inaonyesha meno yenye matundu au yaliyooza, mabaki ya chakula yanaweza kuhifadhiwa kwenye matundu hayo, kuoza, na kutoa harufu
Meno yakitoboka, huweka nafasi ambayo chakula huweza kukaa, na hakiondoki kwa urahisi wakati wa kupiga mswaki. Humo kwenye matundu yaliyoko kwenye meno chakula hicho hushambuliwa na bacteria na hivyo kukiozesha na kuchangia harufu mbaya mdomoni.
Dalili
• Meno yaliyotoboka na yamejaa mabaki ya chakula
• Maumivu ya meno yaliyotoboka
• Maumivu wakati wa kutafuna, au kunywa kitu cha moto au cha baridi
• Jino lililooza kubadilika rangi
• Harufu mbaya kinywani
1.3 Chanzo: Ugonjwa wa kupungua mate kinywani (xerostomia)
Tatizo hili husababishwa na mambo mbali mbali, ikiwemo matumizi ya madawa ya aina mbali mbali mara kwa mara. Madawa mengi husababisha mate kupungua kinywani. Pia magonjwa yanayoshambulia tezi za mate hupunguza mzunguko wa mate kinywani. Mate yana vitu vinavyozuia bakteria kuleta madhara kinywani. Hivyo mate yanapopungua kinywani, hutoa nafasi ya wazi kabisa kwa bakteria walioko kinywani kufanya kazi kwa uhuru zaidi bila kipingamizi ambapo humeng’enya mabaki ya vyakula na kutoa harufu mbaya kinywani
Dalili
• Shida ya kumeza chakula. Chakula kikavu kinakuwa k**a kinakwangua koo la chakula wakati wa kumeza
• Shida ya kuongea kwa muda mrefu kwa sababu ya kinywa kuwa kikavu
• Hisia ya kuwaka moto kinywani
• Kuwa na dalili ya meno mengi kutoboka kwa mara moja
• Kuhisi ukavu kwenye macho
• Harufu mbaya kinywani
1.4 Chanzo: Kutokupiga mswaki vizuri
Picha: Ulimi kuweka mgando mweupe
Kutokupiga mswaki vizuri hupelekea ugavu (dental plaque) kubaki kinywani pamoja na mabaki ya chakula kuwa yamejishika katikati ya meno na hivyo kuoza na kutoa harufu mbaya. Pia mabaki ya ugavu (dental plaque) kwa muda mrefu kwenye meno hupelekea kusababisha ugonjwa wa fizi
Dalili
• Meno kuwa na mgando wa ugaga (dental calculus) wenye rangi ya njano au kijivu, hasa maeneo yanayozunguka ufizi
• Kutoka damu kwa urahisi kwenye fizi hasa wakati wa kupiga mswaki ikiwa hali hii imekuwa ya muda wa siku kadhaa
• Ulimi kuweka mgando mweupe,
• Ulimi ukipitishwa kuzunguka kwenye meno, kunakuwa na hisia za kukosa wororo (sensation of roughness)
• Kutoa harufu mbaya mdomoni
1.5 Kutokusafisha meno ya bandia vizuri
Meno ya bandia ya kuvaa na kuvua (removable partial denture), yanaweza kuhifadhi mabaki ya chakula na ugavu (dental plaque) ambayo hupelekea kutoa harufu yasiposafishwa k**a inavyoelekezwa.
Dalili
• Meno haya huweza hata kusababisha ugonjwa humo humo kinywani unaojulikana k**a “denture stomatitis”, hali ambayo hufanya sehemu zinafunikwa na hayo meno kuvimba, kutoa damu kwa urahisi, na wakati mwingine kuuma na kutoa harufu.
• Pia meno ya bandia ya kugandisha (fixed prosthesis), yakiacha nafasi inaweza kuhifadhi mabaki ya chakula ambacho kikioza huchangia kutoa harufu mbaya mdomoni.
• Ufizi au paa la kinywa (palate) kuvimba na kuuma
2. Tatizo nje ya kinywa
2.1 Chanzo: Magonjwa yanayoathiri mfumo wa hewa
Magonjwa haya yanaweza kuwa kwenye mapafu, kwenye koo, au kwenye uwazi kwenye fuvu la taya unaoitwa “maxillary sinus”. Magonjwa haya yanaweza kusababisha kuongezeka kwa majimaji ambayo yakipata maambukizi hupelekea kutoa harufu mbaya kupitia kinywani
Dalili
• Kuvimba tezi za kinywani
• Kuvimba kooni kunaambatana na maumivu ya kumeza kitu chochote (sore throat)
• Homa kali
• Pua kuziba
• Kutoa mak**asi yenye rangi ya kijani au njano
• Kikohozi kinachoambatana na makohozi
2.2 Chanzo: Magonjwa mengine
Ugonjwa wa kisukari, magojwa yanayoathiri maini,magonjwa ya figo kushindwa kufanya kazi, magojwa yanayoathiri mfumo wa chakula (reflux diseases)
Dalili
• Dalili za ugonjwa wa kisukari: pamoja na hayo mtu huyu hutoa harufu k**a ya matunda kutoka mdomoni mwake
• Dalili za magonjwa ya figo kushindwa kufanya kazi: pamoja na hayo mtu huyu hutoa harufu k**a ya mkojo kutoka mdomoni mwake
• Dalili za magonjwa ya ini, kinywa hutoa harufu inayofanana na harufu ya mtu aliyekunywa pombe anapoamka wakati wa asubuhi
• Dalili za magonjwa ya mfumo wa chakula
3. Ulaji/utumiaji vitu vinavyotoa harufu kinywani
Mfano kula vitunguu (vya kawaida na vitunguu saumu), kutumia kahawa, kuvuta sigara, matumizi ya ugoro, matumizi ya pombe na mvinyo.
Dalili
• Harufu inayofanania na kitu kilichotumika/kinachotumika mara kwa mara mfano vitunguu, kahawa, sigara, ugoro, pombe au mvinyo n.k.
4. Tatizo la kufikirika (psychological/psychiatric illness)
Watu wengine wanakuwa wanaamini kuwa vinywa vyao inatoa harufu mbaya, hali ambayo watu wanaomzunguka hawajawahi kuhisi harufu hiyo kutoka mdomoni. Hali hii ni tatizo la kisaikolojia ambalo mgonjwa anahitaji ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa saikolojia.
Dalili
• Dalili kubwa ni kuwa hakuna harufu yoyote utakayoisikia kutoka kwa mgonjwa huyu, pia ukimchunguza mdomoni, hana tatizo lolote linalosababisha harufu mbaya mdomoni, na hana historia ya ugonjwa wowote unaoweza kusababisha harufu mbaya kinywani
• Katika mazungumzo mtu huyu huonekana kuongelea mambo mengine ambayo hayana mahusiano sana na tatizo lake, pia huweza kuwa na historia ya kuona madaktari wa aina mbalimbali kwa ajili ya tatizo hili bila kupata suluhisho.
Matibabu ya harufu mbaya Kinywani
Unashauriwa kumwona daktari wa afya ya kinywa k**a una tatizo hili au daktari anaweza kugundua jambo hili unapoenda kwa matibabu ya tatizo lingine. Daktari atashirikiana na wewe ili kuweza kujua chanzo cha tatizo kwa ajili ya kulitibu. K**a inavyoonekana hapo juu, ili kutatua tatizo hili inabidi kutibu chanzo cha tatizo.
Namna ya kuzuia tatizo la harufu mbaya kutoka mdomoni
1. Harufu mbaya kutokanana matatizo ya kinywani yanaweza kuzuiliwa kwa urahisi kwa kupiga mswaki kwa usahihi na kusafisha ulimi pia.
2. Meno yaliyo na matundu kuzibwa.
3. Kusafisha meno ya bandia kila baada ya kula, na kuyahifadhi ndani ya maji (kwenye glass au chombo chochote utakachokiandaa) usiku unapoenda kulala katika chombo safi. Kutumia brashi maalumu kutoa chakula kinachojikusanya juu ya jino/meno yaliyogandishwa (k**a yameacha nafasi inayohifadhi chakula).
4. Kufanya uchunguzi wa kinywa na kusafisha meno angalau mara mbili kwa mwaka.
5. Kunywa maji ya kutosha kila siku ili kuupa mwili wako uwezo wa kutengeneza mate ya kutosha
6. Kutumia bazooka isiyokuwa na sukari inasaidia kuhamasisha mate kutengenezwa mdomoni.
7. Kutumia dawa ya kusukutua utakayoshauriwa na daktari wa afya ya kinywa (epuka matumizi holela ya dawa za kusukutua maana zinapatikana kwa urahisi maduka ya dawa, ni vyema ukatumia dawa hii baada ya kumwona daktari wa afya ya kinywa k**a ataona unahitaji atakushauri).
8. K**a chanzo cha tatizo la harufu mbaya ni nje ya kinywa mfano kutokana magonjwa mengine, basi matibabu sahihi ya magonjwa husika yatasaidia kuzuia tatizo hili.